Thursday, April 19, 2012

SABABU SABA ZA KIBIBLIA KWA NINI USIWE MGONJWA.Na. Dickson Kabigumila

                                                                               

Kati ya mambo ambayo yanampa mwanadamu wakati mgumu katika kipindi chake cha kuishi hapa duniani ni swala la kukosa afya…kuwa na udhaifu au kuwa na ugonjwa katika mwili wake.
Ukisoma Biblia inazungumzia habari ya uumbaji wa Mungu hapo mwanzo, na haioneshi hata sehemu moja ya kuwa Mungu aliumba magonjwa,udhaifu au mateso kati ya vitu alivyoumba.

Magonjwa ni matokeo ya anguko la mwanadamu, alipokubali kutomtii Mungu na kumsilkiliza shetani. Akauza haki yake ya kumiliki na kutawala katika maeneo yote (ikiwemo afya).Akamuuzia Shetani haki ya kuwa ‘mungu wa dunia hii’ japo Mungu alimuumba mwanadamu awe ‘mungu wa dunia hii’…yaani awe mwenye kauli ya mwisho hapa duniani kwa niaba ya Mungu aliye hai.
Hata baada ya anguko la mwanadamu, bado Mungu aliweka ‘plan B’ ya urejesho wa kile tulichokipoteza kwa kutokutii kwetu…akaweka SHERIA, KANUNI na TARATIBU ambazo kama zikifatwa kwa usahihi na mwanadamu zitamtoa pale alipo na kumrejesha katika ‘KUMILIKI NA KUTAWALA’ japo si kwa urahisi na wepesi kama kabla ya anguko.
Nilipokuwa ninayapitia maandiko kwa muda wa miaka karibu 9 sasa tangu nilipopata ‘NEEMA’ ya kumjua Yesu kama BWANA na MWOKOZI wangu binafsi…Mungu amenifundisha ‘kweli’ nyingi sana na mojawapo ni hii ya kuwa na ‘AFYA TIMAMU’…Sababu hizi saba za kibiblia zinaeleza ni kwanini uwe na afya timamu(out of sickness and disease phase)…Zinafanya kazi katika maisha yangu…NA HAKUNA WAKATI WOWOTE NINAWEZA KUWA MGONJWA…HAIWEZEKANI NA HAITATOKEA…ni sehemu ya Mpango wa Mungu kwa maisha ya kila mmoja wetu…si kwangu tu…wala kwa baadhi ya watu wenye ‘IMANI KUBWA’ au ‘UPAKO’ sana. Ni kwa ajili yako na ni sasa….!
Ebu tuanze kuzichambua kweli hizi saba, kwa Jina la Yesu:
1.KAZI YA MSALABA
Kama unamwamini Yesu we si mgeni wa neno hilo hapo juu…ina maanisha kufa na kufufuka kwa Yesu…na matokeo yake chanya juu ya maisha yetu.Wengi tunajua Msalaba umetupa kuwa wana wa Mungu, watu wa nyumbani kwa Mungu,umetupa Uzima wa milele,umetupa msamaha wa dhambi nk
Lakini hatuko tayari kukubali kwamba msalaba huohuo umeleta “AFYA YA KIMUNGU” ndani yetu! Biblia ktk 1Petro 2:24 inasema, “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu MWILINI MWAKE juu ya mti ili tukiwa hai kwa mambo ya haki tuwe wafu kwa mambo ya dhambi, NA KWA KUPIGWA KWAKE TULIPONYWA” Haisemi tunaponywa au tutaponywa…inasema ‘TULIPONYWA’ Andiko lingine linatoka katika Mathayo 8:17, “Yeye mwenyewe(Yesu) aliuchukua UDHAIFU wetu, amejitwika MAGONJWA yetu’…kama ameyachukua magonjwa yetu, kwanini sisi(Wakristo) tunayang’ang’ania? kama amejitwika magonjwa yetu kwa nini sisi tunalazimisha kujitwika Magonjwa?

Utamsikia Mkristo aliyeokoka tena kajazwa na Roho wa Mungu lakini anasema…’Yaani hiki kichwa changu kinauma kila mara tangu nikiwa mdogo’…mwingine anasema…’Hili tatizo la kubanwa na kifua ni la familia yetu, hata mama naye analo…’ huku ni kujaribu kukana kile ambacho Yesu alishafanya MSALABANI…ALIYEKUSAMEHE DHAMBI ZAKO NDIYE ALIYEKUPONYA….”Akusamehe maovu yako yote akuponya Magonjwa yako yote” Zab 103:3
Kama unamwamini Yesu…tena kwa moyo wako wote na unasema wewe ni raia wa mbinguni na unadai ya kuwa Mungu ni baba yako…HURUHUSIWI KUWA MGONJWA, DHAIFU hata mara moja…tembea katika afya timamu tangu sasa kwa Jina la Yesu wa Nazareth.
2.WEWE NI NYUMBA YA MUNGU (MAKAO YA MUNGU)
Biblia inasema ya kuwa unapompa Yesu maisha yako na kumwamini, unakuwa ndani yake na Yeye ndani yako wewe, na pia MWILI wako unapata ‘HADHI’ au ‘HESHIMA’ ya kuwa NYUMBA/MAKAZI YA MUNGU ALIYE HAI….”Je hamjui ya kuwa MIILI yenu ni hekalu la MUNGU, na ya kuwa ROHO WA MUNGU anakaa NDANI yengu?” 1Kor 3:16-17, 1Kor 6:14-19
Biblia inaeleza ya kuwa Mungu anakaa sasa ndani ya MWILI wako…kwenye CELLS, TISSUE,ORGANS na System za mwili wako….Je unadhani vimelea vya MAGONJWA vitaweza kuishi katika uwepo wa Mungu uliotuama ndani yako…unaotiririka ndani yako? HAIWEZEKANI NA HAITAWEZEKANA
3.UKO NDANI YA YESU
Biblia inasema katika 2Kor 5:17 ya kuwa “Hata imekuwa mtu akiwa ndani ya Kristo Yesu, ya kale yamepita na tazama yote yamekuwa mapya” Tangu siku ile ulipompa Yesu maisha yako…uliingia ndani yake!
Huo ndo ukweli wa mambo hata kama shetani anajitahidi kukuzuia usilifahamu hili.
Kama ni hivyo, ebu tembea na Ufunuo huu alionipa Mungu nilipokuwa ninafundishwa hili…Ili Ugonjwa uweze kukufikia wewe unapaswa kwanza umtoboe Bwana Yesu, kisha ndio ukufikie na ukupate…kwa hiyo unaamini kuna ugonjwa wenye nguvu ya kumtoboa Bwana Yesu? achilia mbali kuusogelea tu uwepo wake…KUWA NA AFYA NI SEHEMU YA MAISHA YAKO NDANI YA YESU.
4.UMEZALIWA KWA NENO LA MUNGU
Biblia inasema ya kuwa tulio ndani ya Yesu, tumezaliwa mara ya pili(tumeokoka) kwa Neno la Mungu…Soma 1Petro 1:8, Yakobo 1:8… kwa maneno mepesi tu wana wa NENO LA MUNGU….na Biblia inasema ya kuwa NENO ni MUNGU (Yohana 1:1-3)…na kama unataka kupiga hatua yoyote kubwa kiroho au kimwili ni lazima ulitumie NENO na uliishi NENO, yaani uliweke NENO kwenye matendo (Yakobo1:21-24)
Mithali 4:20-22 Inasema, “Mwanangu yasikilize maneno yangu, tega sikio usikilize kauli zangu, zisiondoke machoni pako, uzihifadhi moyoni mwako, maana ni UHAI kwa walio nazo(waliozishika) na AFYA ya mwili wao wote”
5.KUMTUMIKIA MUNGU
Biblia katika KUTOKA 23:25-26 inasema, “NAWE UTAMTUMIKIA BWANA MUNGU WAKO; NAMI nitakibarikia chakula chako na kinywaji chako…SITATIA JUU YAKO MAGONJWA YOTE niliyotia juu ya Wamisri(wasioamini)…kwa maana mimi ni BWANA MUNGU NIKUPONYAYE”
Kama unataka kufurahia afya timamu wakati wote hauna budi kuwa na muda wa kutosha wa kumtumikia Mungu, kwa nguvu zako, fedha au mawazo yako. Na kama ukiwa na bidii katika hili utayapiga teke Magonjwa maishani mwako…Utafurahia AFYA YA KIUNGU kila iitwapo leo!
6.UMEINGIA SAYUNI NA YERUSALEM WA MBINGUNI
Ukisoma katika Isaya 33:21-24 utaona ahadi za ajabu walizonazo wale wanaoishi katika Sayuni…amani, usalama, kumiliki,nk lakini zaidi ni ile iliyoko mstari wa 24 isemayo, “Wala hapana MWENYEJI wa mji huo atakayesema mimi Mgonjwa”…yaani watu wa Sayuni hawana habari ya magonjwa maana Mungu ndiye Mfalme wao na pia ndiye mtetezi wao!
Ukisoma Waebrania12:22 Biblia inasema ya kwamba sisi(tuliokombolewa na Yesu) tumeufikiria mlima Sayuni na Yerusalem wa mbinguni, mji wa Mungu aliye hai, ambako kuna majeshi ya malaika (malaika wa vita/wapiganaji) maelfu elfu…Huku ndiko tuliko, ambapo Mungu ni baba yetu… na sie ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa NYUMBANI KWA MUNGU(Waefeso2:19)
Kama uko ndani ya Yesu, unaishi Sayuni, na HAURUHUSIWI KUWA MGONJWA…maana hapana mwenyeji hata mmoja atakayesema mimi mgonjwa!
7.KAA UWEPONI MWA BWANA
Zaburi 91:1-16 Inasema “Aketiye uvulini(uweponi) mwa aliye juu atakaa salama…Hauaogopa TAUNI(UGONJWA WA MLIPUKO)iliyo gizani wala UELE uharibuo adhuhuri…ijapokuwa watu elfu wataanguka(waakufa kwa sababu ya Magonjwa) mkono wako wa kushoto, naam kumi elfu mknono wako wa kuume,lakini hautakukaribia wewe…maana Bwana atakufunika kwa manyoya yake na chini ya mbawa zake utapata kimbilio…”
Ukitaka kuongeza miaka yako ya kuishi, ukitaka kuwa na Afya ya Kiungu, kulindwa na Nguvu za Mungu, kustawi, kutukuzwa na kuinuliwa na Mungu, yote haya yako katika UWEPO WAKE.

Lazima ujifunze kukaa mbele za Bwana, kupitia maombi, kulisoma NENO, Kumtafakari Mungu, kwa Kusifu na kwa kuabudu pia…TUMIA MUDA WAKO MWINGI UWEPONI KWA BWANA.

Ni maombi yangu kwa BWANA kwamba Mungu aliye hai atayafungua macho ya moyo wako, na Nuru ya Kristo itang’aa ndani yako mara tu umalizapo kuusoma ujumbe huu…Ni ujumbe wa Mungu kwako!
Wako katika Ndani ya Kristo Yesu,

No comments:

Post a Comment