Tuesday, April 24, 2012

JENGA UTHUBUTU MAISHANI MWAKO ILI UNUFAIKE NA FURSA AMBAZO MUNGU ANAKUFUNGULIA.


Kushindwa kuthubutu kumewafanya watu wengi wa Mungu waendelee kutembea katika kiwango cha kawaida katika maisha yao ya kila siku na hata washindwe kuzitumia ...baadhi ya fursa ambazo Mungu anawafungulia kila inapoitwa leo.Ni vema ukafahamu ya kuwa zipo fursa ambazo Mungu atakufungulia katika maisha yako ili akupeleke kwenye kiwango bora zaidi cha maisha ambacho amekukusudia.Lakini hii itategemea uthubutu uliojenga ndani yako wakuziendea fursa hizo bila kuangalia changamoto au upinzani utakaokutana nao.

Ina wezekana ni masomo,ni biashara,ni hali yako ya kiroho,au chochote kile ambacho unatamani kisogee kwenye utukufu mkuu zaidi ambao Mungu ameukusudia kwa ajili yako,napenda nikueleze hili, kama usipoamua kuthubutu na kuchukua hatua ya imani kuziendea fursa hizo kwa ujasiri,amini amini na kwambia,usishangae kuona miezi ikikatika,miaka iikipita na hali yako ikiendelea kuwa palepale.

Ukisoma katika Mk 5:25-34 Utakutana na habari ya Mama aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa na damu kwa miaka takribani kumi na nane,pamoja na kutengwa na jamii yake yote kutokana na tatizo lake hilo,alipoiona fursa iliyobeba uponyaji wake imefunguka,hakujali maneno ya watu wa jamii yake,hakujali aibu ya tatizo lake,hakujali ametafuta jibu la shida yake kwa miaka mingapi ,hakujali watu uliokuwa wanamfuata Yesu walikuwa wengi kiasi gani.Alijenga uthubutu ndani yake ulioambatana na imani yake yakutaka kuligusa vazi la Yesu.Alijitia moyo mkuu na kupenya katikati ya kundi lililokuwa likimsonga Yesu, mpaka alipolikamata pindo la vazi la Yesu na hapo ndipo uponyaji wake ulipo patikana.

Ilikuwa ni lazima alikamate pindo la Yesu ili adake kile alichokuwa anakitafuta.Na hili lisingewezekana kama asingejenga uthubutu na kuamua kuchukua hatua bila kujali changamoto zilizokuwa zikimkabili katika jamii aliyokuwa anaishi.Fikiri kama mama huyu angeendelea kujifungia ndani bila kuchukua hatua nini hasa ingekuwa hatima ya tatizo lake? Ni dhahiri miaka ingekatika huku bado tatizo lake likiwa palepale.

Sikiliza mtu wa Mungu, kama unajua hujaligusa pindo la vazi la Yesu na ndani yako unajua, tena unajua ya kwamba pindo la vazi la Yesu ndio fursa iliyobeba upako wenye majibu unayoyatafuta kamwe usikubali kulala usingizi au kukubaliana na hali uliyonayo.Jitie moyo mkuu katika Bwana, jenga uthubutu ndani yako, usiangalie hali gani ulipitua kabla, usiangalie wanao kuzunguka wanasema nini juu yako,usiangalie umati wa watu unaokusonga katika njia yako.Na kwambia endelea kujipenyeza humohumo kwenye huo umati wa watu,humo humo kwenye hiyo biashara,kwenye hiyo ndoa,kwenye hiyo elimu,kwenye hiyo kazi, haijalishi ulipata hasara mara ngapi,au ulipata upinzania kasi gani.Jenga uthubutu ndani yako na uiendee fursa hiyo,mpaka umehakikisha umeligusa pindo la Yesu.Shaloom!

“Hatukupewa roho ya woga bali ya upendo na nguvu”. <<2Thimotheo 1:7>>

No comments:

Post a Comment