USIPO ITAZAMA FURSA MUNGU ANAYOKUFUNGULIA KWA JICHO LA KIMUNGU NI
RAHISI SANA KUJIKUTA UKIITUMIA VIBAYA,UKIIKATIA TAMAA NA HATA KUTOKUONA MANUFAA
YAKE KATIKA MAISHA YAKO.
Ukisoma katika Mwanzo 25:29-34,
utaona jinsi gani Esau alivyoichezea fursa aliyopewa ya kuwa mzaliwa wa kwanza.Na kwa kutokujua thamani ya fursa ile alijikuta anaiuza kwa ndugu yake tena kwa gharama ndogo ya chakula tu ili atulize njaa iliyokuwa ikimsumbua. Ukitafakari kwa
undani utagundua tofauti kubwa kati ya Esau na Yakobo hususani kwenye jinsi walivyokuwa wakiitazama
fursa ya uzaliwa wa kwanza.Kila mmoja aliitazama kwa jinsi ya kwake,Esau
aliitazama fursa ile kwa jicho la kibinadamu na ndio maana hakuona kile ambacho
Yakobo alikiona.Yakobo aliuona uzaliwa wa kwanza kwa jicho la tofauti,alijua
baraka zilizofungwa ndani ya nafasi ya mzaliwa wa kwanza na ndio maana Esau
alipochezea fursa ile kwasababu ya njaa yake Yakobo aliichangamkia sawasawa bila kupoteza mda.
Macho ya ndani ya watu
yamekuwa na upofu kutokana na kutokukaa vizuri na Mungu.Na hii inapelekea wengi kushindwa kutazitazama fursa zinazofunguliwa katika maisha yao kwa jinsi Mungu anayotaka
wazitazame. Watu wengi wamejikuta wakiuza fursa zinazofunguka maishani mwao kama Esau alivyouza uzaliwa wake wa kwanza tena bila kujua
yakuwa wanachokiuza kinathamani kuu kiasi gani.Esau alikuwa na upofu kwenye macho yake ya rohoni na hivyo hakuona thamani ya uzaliwa
wake wa kwanza na ndio maana haikumpa tabu kuiuza kwa ndugu yake Yakobo.Ukiitazama fursa
kwa jicho la kibinadamu kama Esau, utajikuta ukiiona njaa zaidi kuliko uthamani
na baraka zilizofungwa ndani ya uzaliwa wa kwanza ambazo zinaonwa kwa jinsi ya rohoni pekee.
Ni hasara kiasi gani kuuza fursa
ambayo ingeweza kuamua hatima ya maisha yako kwasababu ya njaa ya kitambo
tu.Leo tunao wakina Esau chungu mzima makanisani na majumbani mwetu, watu wako
tayari kuuza wokovu wao kwasababu ya vitu vya kidunia.Fursa ya wokovu tuliyopewa
tena kwa neema tunaishusha thamani, tunaiuza kama Esau alivyo uza uzaliwa wake
wa kwanza kwasababu ya chakula ambacho ni chakupita tu.Leo hii utakuta mpendwa yuko tayari achezee wokovu
wake na kuanguka dhambini kisa ni hofu ya kuchelewa kuolewa, eti umri umeenda
anahofia atakimbiwa.Leo makanisa yamekuwa kama vitega uchumi,karama na neema
Mungu anazoiachilia bure zinatumiwa kunufaisha matumbo ya watu na familia zao
na si katika kuujenga mwili wa Kristo.
Maombi yangu na dua yangu kwa Mungu, ni Mungu
akatie nuru ndani ya macho ya moyo wako ili ukapate kuona fursa anazokufungulia
kwa jinsi ambayo yeye ameikusudia.Shalooom!
MASSAWE GILBERT
SAA YA WOKOVU NI SASA
No comments:
Post a Comment